Serif
Sans serif
Monospace

bold|normal

-2|-1|N|+1|+2

Mbinu Bora za Uandishi

Ifahamike kuwa kila kampuni ya uchapishaji wa magazeti au vitabu na kampuni za televisheni na redio huwa na mtindo wao wa kuandika au kutangaza habari ambao ni tofauti kidogo na vyombo vingine katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Hata hivyo ziko mbinu ambazo ni za jumla kwa kila mwandishi ambazo hana budi kuzifuata kama kwa mfano matumizi ya tahajia ya maneno, miundo ya sentensi na mpangilio wa maneno. Tofauti zinazojitokeza ambazo hutumiwa na wachapishaji ama wa magazeti au wa vitabu zinazojulikana kama 'House style' ni ndogo na haziwezi kuathiri sana uandishi kwa jumla.

Stephen Maina

Utangulizi

Kwa kuwa waandishi wengi wamesoma katika vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari, imeonekana kuwa kuna haja ya kuwa na mwongozo wa uandishi bora na aina za mitindo inayotumika na kukubalika.

Mwongozo huu umejikita katika matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo msingi katika uandishi wa habari.

Ifahamike kuwa kila kampuni ya uchapishaji wa magazeti au vitabu na kampuni za televisheni na redio huwa na mtindo wao wa kuandika au kutangaza habari ambao ni tofauti kidogo na vyombo vingine katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Hata hivyo ziko mbinu ambazo ni za jumla kwa kila mwandishi ambazo hana budi kuzifuata kama kwa mfano matumizi ya tahajia ya maneno, miundo ya sentensi na mpangilio wa maneno. Tofauti zinazojitokeza ambazo hutumiwa na wachapishaji ama wa magazeti au wa vitabu zinazojulikana kama 'House style' ni ndogo na haziwezi kuathiri sana uandishi kwa jumla.

Maelezo yafuatayo yametokana na utafiti pamoja na ushauriano baina ya wataalamu wa lugha.

Maelezo

Msingi wa maelezo yaliyoandikwa umezingatia miongozo iliyowahi kutolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) siku za nyuma kama ilivyoandikwa katika machapisho yao kama kitabu cha "Jifunze Kiswahili Uwafunze Wengine,' pamoja na 'Mwongozo wa Uandishi'.

Kwa kuanzia ningependa kufafanua baadhi ya maneno yanayokanganya kiasi fulani wasomaji wengi kutokana na kushindwa kuyapambanua. Sababu kubwa ya mkanganyiko huu ni athari ya lugha za asili katika Kiswahili sanifu pia ni misingi mibovu wa sarufi ya Kiswahili inayosababishwa na walimu wa shule za msingi wasiokuwa na ujuzi wa kutosha katika taaluma katika fani ya Fonolojia, Fonetiki, Mofolojia, Semantiki na Sintaksia. Pia wako wale wanaoathiriwa na lugha za kigeni kama Kiarabu na Kiingereza. Lugha hizi za kigeni kimetufanya tuione lugha ya Kiswahili kama chotara wa lugha nyingine wakati lugha hii ina misingi ya lugha ya Kibantu. Nitaanza kufafanua baadhi ya maneno nna vifungu vya maneno kwa utaratibu wa kutumia alfabeti. Kwa mfano:

A

Ajali/ajari:

Ajali ni tukio lenye madhara yanayotokea ghafla. Ajari ni malipo kwa kazi ya ziada na jina linalofahamika ni ovataimu ambalo limetoholewa kutoka katika neno la Kiingereza la 'overtime'.

Aidha/au/ama:

Neno aidha asili yake ni Kiarabu na tangu likopwe, matumizi yake hayajabadilika. Kuna wakati tunalitumia kama waaidha. Watumiaji wengi wanafuata mtindo wa Kiingereza wa 'either ... or'. Tunasoma kwa mfano: "Wataalamu wa Kichina watabaki aidha bara au visiwani. Matumizi sahihi ni "Wataalamu wa Kichina watabaki ama bara au visiwani. Maana ya aidha ni tena, basi, zaidi ya hayo, vilevile. Kwa mfano: Kabla ya kwenda sokoni nitapitia aidha benki kuchukua fedha.

Ahirisha/hairisha:

Neno sahihi ni ahirisha. Kuahirisha maana yake ni kuchelewesha jambo kwa makusudi ili lifanyike baadaye.

Adhima/azma:

Neno adhima si neno sahihi la Kiswahili ila liko neno adhimisha ambalo maana yake ni kufanya sherehe ya kukumbuka kwa tukio fulani kama vile siku ya kuzaliwa, siku ya kufunga ndoa, siku ya kupata uhuru, n.k. Neno lingine linalofanana na hilo ni adhimu ( kiv) –enye sifa, iliyotukuka, tukufu, jalili. Azma ni jambo linalokusudiwa kufanywa, makusudio au lengo. Wakati mwingine huandikwa kama azima.

Alimradi/ilimradi:

Haya ni maneno yenye maana moja. Maana yake ni ili, iwapo, kwa masharti kwamba, mradi.

Aidha:

Maana ya aidha ni vilevile, pamoja na hayo, pia, isitoshe n.k. Kuna wakati tunachanganya aidha na au katika sentensi moja. Hii inatokana na athari ya Kiingereza ya kutumia 'either … or'... Kwa usahihi inatakiwa iwe 'ama / au' tunapotaka kulinganisha mambo.

B

Budi:

Neno hili likisimama peke yake lina maana ya hiari. Tukisema ,"Wakulima ni budi walime" tuna maana kuwa wakulima ni hiari walime. Tunatakiwa kusema "Wakulima ni lazima walime au wakulima hawana budi kulima. Kwa usahihi tunasema "Wakulima hawana budi kulima" (yako maneno yanayofanana kimuundo kama sina budi, hatuna budi, hawana budi , huna budi)

Baadaye/baadae:

Neno sahihi ni baadaye

D

Digiti/Digitali:

Digiti ni nomino na limetoholewa kutoka kwa neno 'digit' lenye maana ya tarakimu. Neno hili ni nomino na ni sahihi. Digitali ni kisifa (adjective). Kwa kawaida tunatohoa nomino na wala siyo kisifa. Hivyo neno sahihi ni 'digiti".

Durusu/rudufu:

Haya ni maneno yanayochanganywa na yana maana tofauti. Kudurusu ni kupitia tena maandishi yaliyoandikwa kwa madhumuni ya kusahihishwa au kuboreshwa na kutoa toleo jipya. Rudufu ni kufanya nakala, kufanya kitu madhubuti k.v kurudufu nyuzi kuwa imara.

Darubuni:

Ni chombo cha kuonea mbali; kionea mbali yaani 'Telescope/binoculars'.

Dahili/sajili:

Maana ya kudahili ni kutaka kujua habari za watu kwa kuulizauliza au kudadisi. Kusajili ni kuweka orodha ya kumbukumbu za vitu au watu kwa kuviandika katika daftari maalumu.

F

Fedha/pesa/hela:

Haya ni maneno yenye maana moja lakini yana asili tofauti. Maneno mengine yanayofanana na hayo ni sarafu, fulusi, faranga ambayo hutumika katika malipo. Maneno yote yanakubalika. Hata hivyo tuna mazoea ya kutumia neno fedha upande wa bara na pesa upande wa visiwani.

Fikiri/dhani:

Maneno haya yanafanana kwa kiwango fulani lakini wengi wetu huyachanganya na kuyatumia kama visawe. Yana tofautiana kidogo. Fikiri ni kutumia ubongo kutatua jambo, kutafakari, kuwaza. Kudhani ni kufikiri bila kuwa na uhakika.

G

Ghairi:

Kuacha kutenda kilichokusudiwa.

Ghushi/gushi:

Neno sahihi ni ghushi.

H

Hadubini:

Ni chombo cha kuona vitu visivyoonekana kwa macho (Microscope).

Hoteli/mahoteli:

Neno sahihi ni hoteli.

Hovyo/ovyo:

Neno sahihi ni ovyo.

Hadhari/Tahadhari:

Hadhari ni nomino na tahadhari ni kitenzi. Hadhari ni uangalifu. Hadhari kabla ya athari/hatari. Tahadhari ni kitenzi. Kuepuka jambo ili usipatikane na hatari au ubaya.

Hatima/hatma:

Neno sahihi ni hatima.

Harusi/arusi:

Maneno yote mawili yanatumika ila kwa mazoea ya wengi neno harusi ndilo linalotumika zaidi.

I

Idadi/nambari:

Idadi ni jumla ya vitu au mambo yanayohesabika. Nambari limetokana na neno namba (number) yana maana ya tarakimu kama 1, 2, 3, 4, 5. Idadi ni namba au hesabu ya kujumuisha. Tunasema idadi kubwa ya Watanzania ni wakulima.

J

Jingine/Lingine:

Yote ni sahihi ila hutegemea muktadha husika.

Jinsi na jinsia:

Jinsi ni namna kitu kilivyo au kiumbe kama vile binadamu, wanyama au ndege. Tunayo jinsi ya kike na jinsi ya kiume. Kwa lugha ya kigeni ni 'sex'. Jinsia ni hali ya kuwa mume au mke. Masuala yanayohusiana na mwanamume na mwanamke. Kwa lugha ya kigeni ni 'gender'.

K

Kuwapo/Kuwepo:

Neno linalosadifu ni kuwapo ijapokuwa kwa mazoea watu wengi wanatumia kuwepo.

Kiwanda/Karakana:

Kiwanda ni mahali penye sehemu za kuundia vitu mbalimbali kama milango, vioo, madirisha, magurudumu, n.k. Sehemu hizi hufahamika kama karakana. Hivyo kiwanda huwa ni mkusanyiko wa karakana mbalimbali.

Kampuni/Makampuni:

Neno sahihi ni kampuni na wala siyo makampuni.

Kurudufu:

Maana yake ni kunakili au kutoa nakala nyingine.

Kimbiza/Wahisha:

Kukimbiza ni kufuata kitu au mtu kwa mbio nyuma au kufukuza. Kuwahisha ni kutenda jambo mapema kabla halijaharibika. Waandishi wanatumia 'kukimbiza badala ya kuwahisha.

Kuongea/kuzunguma:

Tofauti kati ya maneno haya ni ndogo sana. Kuongea ni kushiriki katika mazungumzo. Kuzungumza ni kusema maneno katika mkutano au kwenye mjadala au baraza na kutoa maoni.

Kupeleka ni kuchukua kitu au mtu na kukifikisha/kumfikisha mahala fulani. Tukiongeza kiambishi cha –ea tunapata kupelekea kwa maana ya kufikisha kitu kwa niaba ya… Mtoto alimpelekea mzazi wake mbegu shambani. Hivi sasa matumizi ya pelekea yanaleta kichefuchefu kwa Waswahili.

Kuyeyuka/kuyayuka:

Neno sahihi ni yeyuka kwa maana ya kugeuka kwa kitu kigumu kuwa kioevu.

Kunyauka/kukauka:

Kunyauka ni kufifia kwa sababu ya ukame au joto. Kukauka ni kutoka maji na kuwa kavu.

Kengeuka:

Kwenda kombo, angamia. Kengeua ni kumfanya mtu afuate njia mbaya au tabia mbaya, kupotosha.

Kutokana/Kufuatia:

Maneno haya mawili yanatumika kama vile yana maana moja. Kwa kweli yana maana tofauti kabisa. Kwa mfano tunasema," Kutokana na njaa kali inayowakabili wananchi wa Bariadi, serikali imepeleka magunia 20,000 ya mahindi. Ni makosa kusema, " Kufuatia njaa kali inayowakabili wananchi wa Bariadi, serikali imepeleka magunia 20,000 ya mahindi.

Kugharamia/kugharimia:

Neno sahihi ni kugharimia badala ya kugaramia. Gharama ni nomino.

Kwa ujumla/kwa jumla:

Maneno yote yanatumika kutegemeana na maudhui. Tunasema kwa jumla maisha ni magumu. Hata hivyo neno linatumika kama: Kwa ujumla wake mvua imekithiri. Ni makosa kutumia, 'Kwa ujumla tumefanikiwa… bali kwa jumla tumefanikiwa.'

L

Loga/roga:

Maneno yote yana maana moja. Maana yake ni kudhuru kwa uchawi kwa kutumia vifaa aina ya sihiri, hirizi, kago, azima au amali). Hata hivyo neno lililozoeleka zaidi ni roga.

M

Mazishi/Maziko:

Maneno haya yanatokana na shina moja la 'zika' lakini yana matumizi tofauti. Maziko ni kitendo cha kuzika maiti. Tupokwenda mazikoni tunakwenda makaburini kuzika. Tunakwenda kuhudhuria anakozikwa maiti. Mazishi ni matayarisho kabla ya maziko kama kutafuta vifaa, kuchimba kaburi. Pia baada ya kuzika kuna matanga na ada zake kama ufanyaji wa hesabu zilizotumika. Maziko yana muda maalumu wakati mazishi hayana muda maalumu. Ni matayarisho tu ya kutekeleza kitendo cha kuzika.

Msiba:

Jambo au tukio linalomfanya mtu awe na huzuni, kilio k. v. kufiwa.

Masurufu/Marupurupu:

Masurufu (Imprest) ni fedha anazopewa mtu aendapo safarini kwa ajili ya matumizi ya huko aendako. Mhusika anaporudi hudaiwa stakabadhi kuonyesha fedha hizo alivyozitumia. Marupurupu (Allowance) ni fedha za ziada anazopewa mtu mbali na mshahara wake. Fedha za marupurupu huweza kuwa ni malipo ya ajari (ovataimu) na una mamlaka nazo. Hudawi stakabadhi. Malipo mengine ambayo huhitaji stakabadhi ni posho ya jamala, posho ya kijikimu, posho ya takrima, posho ya usumbufu, n.k.)

Majira:

Maana ya majira ni kipindi maalumu cha hali ya hewa. Neno jingine ni msimu. Kuna majira ya mvua, majira ya kiangazi. Maana nyingine ni mwendo wa kawaida wa saa. Kwa mfano, saa yangu imepoteza majira. Ni makosa kuandika majira ya saa bali ni sahihi kutumia neno saa tu.

Mkasa/Maafa:

Maneno haya hudhaniwa kuwa ni sawa lakini yana maana tofauti. Mkasa ni neno linahusiana na tukio au jambo la huzuni au la kushtua. Maafa maana yake janga, balaa na pia msiba. Kwa mfano kijiji kinaweza kupatikana na maafa ya mafuriko au nyumba kuteketea kwa moto.

Mtaalamu / Mtaalam:

Neno sahihi ni lile lililoishia na 'u' yaani mtaalamu.

Mtaala/mtalaa:

Watu wengi wamezoea kutumia mtaala lakini sahihi ni mtalaa.

Mashtaka/ Mashitaka:

Neno sahihi ni mashtaka

Makala haya / Makala hii:

Sahihi ni makala haya.

Muafaka/mwafaka:

Neno sahihi ni mwafaka.

Mkristo/Mkristu:

Maneno yote mawili ni sahihi na hutegemea dhehebu husika.

Mtazamo/Mtizamo:

Neno sahihi n mtazamo kutokana na neno tazama na wala siyo mtizamo.

Maskini/Masikini:

Neno sahihi ni maskini.

Makandarasi/Wakandarasi:

Neno sahihi ni makandarasi.Matanga n mkusanyiko wa watu kwenye nyumba ya mfiwa ili kuomboleza na kuwaliwaza wafiwa-huwa siku chache baada ya kuzika.

Mwongozo/muongozo:

Neno sahihi ni mwongozo.

Mashaka/Shaka:

Haya ni maneno mawili yenye maana tofauti. Maana ya mashaka ni mambo magumu yanayomfika mtu, tabu, dhiki, adha. Shaka ni wasiwasi, hali ya kutokuwa na hakika ya jambo, hatihati.

Mwereka/Mweleka:

Neno sahihi ni mwereka.

Mahabusu/mahabusi:

Mahabusu ni mahali ambapo watu wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali huwekwa.

Mahabusi:

Ni watuhumiwa wanaosubiri kesi zao kuhukumiwa. Hata hivyo, imezoeleka kimakosa kwa watuhumiwa kuitwa mahabusu.

Masilahi na Maslahi:

Neno sanifu ni masilahi.

N

Neno lingine/neno jingine:

Matumizi sahihi ni neno lingine.

O

Ofisa/afisa:

Neno sahihi ni ofisa lililotokana na utohozi wa neno 'officer'.

Ovyo/hovyo:

Sahihi ni ovyo.

Onesha/ Onyesha:

Neno sahihi ni kuonesha. Onesha shina lake ni 'ona.' Kuona ni kutambua kitu kwa kutumia macho. Onyesha chimbuko lake ni 'onya.' Kuonya ni kuasa au kuhadharisha.

P

Pasa/Pasha:

Maneno haya yanakaribiana katika matamshi lakini iko tofauti kubwa sana katika maana. Maana ya pasa ni kuwajibika, kulazimika. Nawajibika kuitunza familia yangu yaani inanipasa kuiangalia familia yangu.

Pasha:

Maana ya pasha ni kusababisha kupata kitu au kuenea kwa kitu. Tunapasha habari, tunapasha moto. Kupashana habari ni kueneza taarifa au kutangaza.

Pokea/pokelea:

Kwa mujibu wa sarufi ya Kiswahili unaweza kufanya kitendo fulani kwa ajili ya au kwa niaba ya mtu mwingine. Kwa hiyo, kupokelea ni kupokea kwa niaba ya mtu mwingine. Kwa hali hii mgeni hupokewa na wala hapokelewi. Ni makosa kusema Rais wa nchi amepokelewa bali amepokewa kwa shangwe na vigelegele. Kupokea ni kupata kitu kutoka kwa mtu mwingine, kukaribisha au kulaki.

Pelekea/Sababisha:

Kupelekea ni neno linalotumika badala ya kusababisha. Neno kusababisha linatakiwa kutumika badala ya kupelekea.

Pacha/mapacha:

Neno sahihi ni pacha.

Padri/padre:

Neno sahihi ni Padri.

R

Rufaa/rufani:

Yote yanatumika na ni sahihi.

Rangi ya njano/rangi ya manjano:

Ni mazoea ya watu wengi kutumia manjano badala ya njano lakini yote ni sahihi.

Rundo/Lundo:

Neno sahihi ni rundo (mrundikano). Lugha za asili zinatupotosha tunapochanganya /L/ na /R/ na kupata lundo.

S

Saini/sahihi:

Neno saini limetoholewa kutoka katika neno la Kiingereza la 'sign'. Huko linatumika kama nomino au kitenzi. Waswahili walipolitohoa wamelitumia kama nomino tu. Neno saini linapotumika kama kitezi linakosewa. Kwa mfano: "Uingereza na Tanzania wamesaini mkataba wa shilingi 300 milioni kwa ajili ya kuimarisha elimu nchini." Kwa usahihi ingepaswa kuandikwa maneno 'kutia saini' na siyo kusaini.

Swala/sala:

Haya ni maneno yanayotumika katika ibada. Kwa Waislamu wanatumia swala na kwa Wakristo ni sala.

Sheria/sharia:

Sahihi ni sheria ambalo limesanifiwa na Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ijapokuwa huko Zanzibar, bado neno sharia linaendelea kutumiwa.

Soko/gulio:

Soko maana yake ni mahali penye mkusanyo wa watu wengi wanaonunua bidhaa rejareja. Gulio ni soko lifanywalo shughuli zake mara moja kwa juma. Neno linalofanana na soko ni chete. Kwa hiyo chete na gulio yana maana inayofanana kwani hufanyika mara moja kwa juma ambapo soko hufanyika kila siku au baada ya siku moja au mbili.

Shule/skuli:

Kwa upande wa Bara neno lililozoeleka ni shule. Lina asili ya Kijerumani 'schule' na halina wingi. Ni makosa kutumia mashule. Huko Zanzibar neno linalotumika ni skuli badala ya shule. Limetoholewa kutoka kwa neno 'school' lenye asili ya Kiingereza.

Shaka ni hali ya kutokuwa na uhakika wa jambo, kuwa na wasiwasi, hatihati, wahaka. Wengi hulichanganya na neno mashaka ambapo mashaka linaeleza hali inayoashiria mambo magumu yanayomfika mtu katika maisha, tabu, dhiki, adha, n.k.

Shehe/Shekhe/Sheikh:

Maneno Shehe au Shekhe ndiyo yaliyo sanifu lakini siyo sheikh.

T

Tuma/Peleka:

Kutuma hutumika kwa maana ya kupeleka. Kutuma ni kuagiza, kuamuru au kumtaka mtu (siyo kitu) afanye jambo. Kwa mfano:

Tahayari/tahayuri:

Tahayari ni kitenzi na maana yake ni kuona haya baada ya kutenda au kufikwa na jambo la fedheha, ingiwa na soni.

Tahayuri ni nomino na ni hali ya kuona haya baada ya kutenda au kufikwa na jambp la fedheha.

Tegemea/Tarajia/Tazamia:

Maana ya kutegemea ni kushikilia, kuegemea au kuzuilia. Kutarajia au kutazamia ni kutumainia kupata/fanya jambo.

Tizama/Tazama:

Neno sahihi ni tazama.

U

Uamuzi/Maamuzi:

Neno uamuzi ni sahihi na siyo maamuzi.

Uchaguzi/chaguzi:

Uchaguzi ni namna ya kutenga kitu kinachofaa na kisichofaa. Pia ni upagaji kura. Kwa maana hiyo neno chaguzi linatumika kimakosa.

Neno uchaguzi ni sahihi na halina wingi ila wako wanaolazimisha kulitumia kama chaguzi.

Vivyo hivyo kwa neno tafiti. Halipo neno tafiti bali neno sahihi ni utafiti. Haya ni makosa.

Upungufu/Mapungufu:

Neno sahihi ni upungufu na wala siyo mapungufu.

Uzito/uzani:

Maneno haya yana maana sawa kwa maana ya hali ya kuelemea. Hata hivyo uzito una maana nyingine ya ziada. Kwa maana hiyo uzito maana yake ni kuwa na umuhinu wa jambo. Kwa mfano: Serikali imeweka uzito katika suala la kuongeza uchumi.

Ujumbe/jumbe:

Ujumbe ni taarifa, habari, salamu. Pia mtu au kundi la watu linalopeleka habari kwa mtu/watu fulani. Jumbe ni mkuu wa mji au mtaa.

Ushirikiano/Mashirikiano:

Neno sahihi ni ushirikiano. Mashirikianao linatumika kimakosa.

V

Vyema/vema:

Neno sahihi ni vyema.

W

Waislamu/Waislam:

Sahihi ni Waislamu.

Warsha/Kongamano:

Warsha ni mahali ambapo wataalamu hujumuika ili kujadili masuala kadhaa ya kitaalamu. Katika warsha wataalamu hugonganisha vichwa na mwisho hutoa kitu fulani. Kongamamo ni mkusanyiko wa watu wanaojadili jambo fulani. Watu hupeana mawazo katika kujadili jambo fulani la kuelimishana.

Wakala/wakili:

Wakili linatokana na kitenzi wakilisha. Kuwakilisha ni kusimamia jambo kwa niaba ya mwingine. Neno wakili hutumika katika kesi. Tumesikia watu wakisema kazi ya wakili ni kumtetea mshtakiwa. Wakala ni kitu au chombo chenye madaraka katika kusimamia jambo fulani. Hapa nchini tuna wakala wa meli, wakala wa biashara ya mazao, n.k.

Wasilisha/Wakilisha:

Maneno haya yanatofautiana katika maana. Kuwasili maana yake ni kufika mahali. Wasilisha ni kufikisha kitu mahali fulani. Wakilisha linatokana na wakili kwa maana ya kufanya jambo kwa niaba ya mtu mwingine. Ni makosa kusema kuwa, 'Juma amewakilisha barua ofisini' bali amewasilisha barua ofisini.

Wasia/Wosia:

Wasia ni maagizo ya mtu kwa watu wake ambayo wanatakiwa kuyafuata iwapo atakufa au ataondoka. Neno jingine ni usia. Neno wosia siyo Kiswahili sanifu.

Wehuka/weuka:

Neno linalotumika ni wehuka. Linatokana na jina wehu kwa maana ya kutokuwa na akili timamu. Hali ya kukaribia kuwa uwenda wazimu.

Wahisha ni kutenda jambo kabla halijaharibika. Wengi wetu tunayachanganya kumbe yana maana tofauti kabisa. Ni sahihi kusema kuwa tunamwahisha mgonjwa hospitali na wala siyo 'tunamkimbiza' mgonjwa hospitali.

Y

Yoyote/yeyote:

Tofauti za maneno haya hutegemea muktadha. Tunasema mtu yeyote lakini tunasema mazingira yoyote.

Ni matumaini yangu kuwa msomaji atakuwa amepeta ufafanuzi wa maneno yanayokanganya ili awe na msimamo thabiti wa lugha ya Kiswahili.

Источник: http://www.mwananchi.co.tz/(1) | http://www.mwananchi.co.tz/(2)