Lugha ya Kiswahili ni kiungo muhimu sana katika maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki hasa katika uchumi, elimu, siasa, maendeleo ya Kiswahili, utamaduni, biashara, n.k. Hivi sasa ziko juhudi za ushirikiano na maelewano kwa jamii nzima ya Afrika Mashariki kupitia lugha ya Kiswahili.
Nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki yaani Burundi, Kenya, Tanzania, Rwanda na Uganda ziko katika harakati za kuboresha muundo wa jumuia hii kwa kuangalia upya majukumu yake baada ya kuvunjika kwa Jumuia ya Afrika Mashariki takriban miaka 20 iliyopita. Idadi ya wanachama imeongezeka kutoka nchi tatu za Kenya, Tanzania na Uganda na kuwa nchi tano baada ya nchi za Rwanda na Burundi kujiunga na Jumuia hii.
Mojawapo ya mambo muhimu yaliyokubaliwa na viongozi wa nchi hizi yalihusu suala zima la lugha ambalo litasaidia kurahisisha mawasiliano baina ya wananchi wa nchi hizi kuanzia ngazi za chini kwa wananchi wa kawaida hadi ngazi ya juu kwa viongozi wakuu. Lugha ya Kiswahili ilipewa nafasi kubwa ya kuweza kutumika kama lugha ya mawasiliano miongoni mwa nchi zote za Jumuia hii.
Itakumbukwa kuwa wakati wa enzi ya ukoloni wa Uingereza ilikuwapo kamati ya lugha ya nchi za Afrika Mashariki iliyojulikana kama Kamati ya Lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki. Lugha ya Kiswahili ilipewa nafasi kubwa tangu mwaka 1930 wakati kamati ilipoanzishwa hadi mwaka 1964 kamati ilipovunjika. Kamati ilipovunjika mwaka 1964 baada ya kila nchi kupata uhuru wake, Tanzania ndiyo iliyokuwa mwenyekiti wa mwisho wa kamati na hivyo kuendelea kutekeleza baadhi ya majukumu ya Kamati hadi leo chini ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ambayo iko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) imefanyiwa mabadiliko ya muundo wake kiutendaji na sasa inafahamika kama Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI). Taasisi ya TATAKI sasa imekuwa ni muunganiko wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili na Idara ya Kiswahili zote cha Chuo Kikuu cha UDSM. Idara ya Kiswahili iliyokuwa inajishughulisha na ufundishaji wa Kiswahili kwa wanachuo wa digrii ya kwanza, ya uzamili na uzamivu.
Kamati ya Lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki ilikuwa na utaratibu wa kukutana kwa zamu katika nchi wanachama kama ifuatavyo:
Tangu mwaka 1964 baadhi ya shughuli za kamati ziliendelea kusimamiwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). Kutokana na kila nchi kupata uhuru wake, mfumo wa sera ya lugha uliachwa nchi wanachama jukumu la kuendeleza lugha ya Kiswahili. Mwaka 1967 Tanzania ilianzisha Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) kwa lengo la kukuza, kuendeleza na kuratibu maendeleo ya Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majukumu ya Bakita yalitekelezwa vilivyo hasa suala la kusanifu lugha ya Kiswahili na kutayarisha istilahi za masomo mbalimbali kama Kemia, Fizikia, Hisabati, Utawala, Siasa, Elimu, n.k. Hatua ya pili ni kutayarisha kamusi za istilahi hizi kazi ambayo imekamilishwa na TUKI.
Mwaka 1970 TUKI iliwekwa chini ya mamlaka ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati kilipoanzishwa rasmi. Hadi sasa taasisi hii iko chini ya chuo hicho.
Mwaka 1999 viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki walikutana na kuona umuhimu wa kuwa na chombo kimoja rasmi ambacho kazi zake ni kukuza, kuendeleza na kuratibu Kiswahili katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla. Chombo hiki kinajulikana kama Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki chenye malengo ya kuwezesha kukuza siasa, uchumi, maendeleo ya jamii, elimu, utamaduni, sayansi na teknolojia katika eneo la Afrika Mashariki.
Dira ya Kamisheni hii ni kuwa chombo mahususi cha kukuza, kuratibu na kuendeleza Kiswahili kwa ajili ya maendeleo ya uchumi, siasa, utamaduni, elimu kwa nchi wanachama.
Makao Makuu wa Kamisheni hii yatakuwa Zanzibar na mipango ya kuwapata viongozi wa Kamisheni inaendelea.
Mojawapo ya shughuli za Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ni kusanifu maneno mapya pamoja na kuoanisha maneno ya zamani ili yatumike kwa ajili ya kuimarisha maelewano baina ya nchi zote za Jumuia ya Afrika Mashariki. Kikwazo kilichokuwapo hapo awali ni kutoikuza lugha ya Kiswahili kwa kiwango cha kimataifa kwa upande wa taaluma ya sayansi na kiteknolojia. Bingwa na mtaalamu aliyebobea katika Kiswahili Profesa Ali Mazrui aliwahi kusema kuwa sera ya elimu na ya lugha ya Kiswahili havikupewa kipaumbele katika ukuzaji wa sayansi na teknolojia. Ukosefu wa istilahi za Kiswahili katika sayansi na teknolojia umesababisha walimu na wahadhiri kupata matatizo katika kuandika vitini na vitabu vya sayansi kwa lugha ya Kiswahili.
Kihistoria nchi za Kenya na Uganda zimetegemea sana istilahi zilizotayarishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), Taasisi ya Ukuzaji Mitalaa (TIE), Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE) na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).
Hata hivyo, katika ngazi ya vyuo vikuu, wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vikuu vya Kenya, wamekuwa na mawasiliano ya karibu ya kitaaluma baina yao kwa kubadilishana taaluma mbalimbali. Mfano mzuri ni wakati UNESCO/SIDA walipofadhili semina kuhusu masuala ya usanifishaji wa istilahi za Kiswahili mwaka 1989. Wanataaluma wengi kutoka Kenya walihudhuria semina hii na huu ukawa ni mwanzo nzuri wa ushirikiano katika kukuza lugha ya Kiswahili kwa kiwango cha vyuo vikuu.
Inasemekana kuwa watumiaji wa istilahi za Kiswahili ni kwa ajili ya wanataaluma na si kwa watu wa kawaida. Kwa hiyo wataalamu wanaotaka kuandika vitabu au vitini vya kufundishia masomo ya sayansi wanazo istilahi za kuwawezesha kukamilisha azma zao. Wataweza kutumia istilahi zilizotayarishwa na Bakita na kuchapishwa katika kitabu cha Istilahi za Kiswahili cha mwaka 2005 na machapisho mengine yanayoweza kupatikana Bakita na Tuki. Iko mifano michache ya wanataaluma wa masomo ya Kemia na Hisabati waliowahi kuandika miswada ya masomo hayo kwa Kiswahili katika kiwango cha elimu ya kidato cha tano na sita wakitumia istilahi ambazo zimetayarishwa na Bakita. Kwa bahati mbaya wachapishaji wa vitabu walishindwa kuchapisha miswada ya vitabu hivyo kutokana na kutokuwapo kwa sera kamili ya lugha ya Kiswahili katika shule za sekondari.
Bakita walitayarisha istilahi za aina mbalimbali kwa kutumia njia zifuatazo:
Kiingereza | Kiswahili |
---|---|
atom adapter battery speaker transformer |
atomi adapta betri spika transfoma n. k. |
ship capital plans equality |
meli mtaji mpango usawa n. k. |
prehistory labour force appendix triangle back sight fungicide boar saw |
historiakale nguvukazi kidoletumbo pembetatu kipimonyuma kiuakuvu nguruwedume nguruwejike n. k. |
Hii ni mifano michache ambayo imetumika katika kuongeza istilahi za Kiswahili katika juhudi za kupata maneno mapya ya sayansi. Inawezekana ziko njia nyingine ambazo wataalamu wetu wa Kiswahili watabuni ambayo yatasaidia kukifanya Kiswahili kiweze kumudu maendeleo ya sayansi na teknolojia. Jambo la msingi ni kwa serikali kutoa fedha za kutosha kwa watafiti wa lugha ya Kiswahili kuweza kufanya utafiti wa kina katika lahaja za Kiswahili kama Kiamu, Kingazija, Kitumbatu, Kihadimu, Kimvita, n.k. pamoja na lugha zetu za asili ambazo ni hazina kubwa katika ukuzaji wa Kiswahili.
Kwa mujibu wa Sera ya Elimu ambayo imetoka hivi karibuni, upo mpango wa muda mfupi, wa kati na muda mrefu wa kukiwezesha Kiswahili kuwa ni lugha ya kufundishia katika mfumo mzima wa elimu kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu. Lengo ni kuhakikisha kuwa masuala ya sayansi na teknolojia yanapata nafasi yake katika maendeleo yetu kwa kutumia Kiswahili. Maandalizi yanayotakiwa kufanywa ni kama kuandika vitabu na vifaa vingine vya kujifunzia na kufundishia na pale inaposhindikana kutafsiri kutoka lugha za kigeni. Pia kuwaandaa walimu hata wale wa kigeni watakaokuja kufundisha hapa nchini . Suala la msingi ni kwa viongozi wetu kubadilika kifikra na kuona kuwa kukitumia Kiswahili si kujidhalilisha bali ni kupiga hatua kimaendeleo katika sayansi na teknolojia kwa taifa letu. Matumizi ya lugha za asili katika elimu ni dhana inayokubalika kwa nchi nyingi duniani kama vile Kenya. Je, ni nini mwelekeo wa Tanzania?
Источник: http://www.mwananchi.co.tz/